Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

ad728

FUTURE WORLD VOCATION INSTITUTE YAZIDI KUFUNGUA MILANGO YA FURSA KWA VIJANA

Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Chama cha ACT-Wazalendo, Mhe. Bakari Shingo akizungumza na madeleva wanaopata mafunzo  katika Chuo cha Ufundi Stadi Future World Vocation Institute kilichopo Chanika kwa Ndevu, leo Septemba 25, 2026 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Future World Vocation Institute, Robert Mkola (kushoto) akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Chama cha ACT-Wazalendo, Mhe. Bakari Shingo wakati alipotembelea chuo hicho 

Mkuu wa Idara ya Masoko Future World Vocation Institute, Chanika kwa Ndevu David JF Msumba akizungumza jambo na mwalimu  wa chuo hicho.

...............

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAAM

Madereva nchini wametakiwa kuongeza ujuzi kwa kurejea katika vyuo vya ufundi na mafunzo ya udereva ili kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia ya magari na kuimarisha usalama barabarani.

Akizungumza leo Septemba 25, 2026 jijini Dar es Salaam na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Future World Vocation Institute kilichopo Chanika kwa Ndevu, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Mhe. Bakari Shingo, amesema kuwa maendeleo ya teknolojia yamebadilisha kwa kiasi kikubwa mifumo ya magari ikilinganishwa na magari yaliyotumika miaka ya nyuma.

Mhe. Shingo amesema kuwa madereva wanapaswa kuendelea kujifunza ili kuendana na mabadiliko hayo, huku akisisitiza kuwa mafunzo ya mara kwa mara yana umuhimu katika kuongeza uelewa wa madereva kuhusu uendeshaji wa magari ya kisasa, kanuni za usalama barabarani pamoja na matumizi sahihi ya teknolojia zilizopo kwenye vyombo hivyo.

“Magari tuliyokuwa tukiyaendesha miaka iliyopita siyo yaliyopo sasa. Teknolojia inabadilika kila siku, hivyo dereva anapaswa kuendelea kujifunza ili aweze kuendesha gari kwa uelewa na usalama zaidi,” amesema Mhe. Shingo

Amesema awali alipokea hoja kutoka kwa baadhi ya madereva wenye leseni daraja C kwamba hawakuona umuhimu wa kurejea darasani, lakini baada ya kupata maelezo kuhusu mabadiliko ya teknolojia na umuhimu wa mafunzo, amebaini kuwa elimu ya ziada inaweza kuwa na mchango katika kuboresha utendaji wao.

Mhe. Shingo amewataka vijana wanaojihusisha na udereva wa bodaboda kutumia fursa zilizopo kujifunza ujuzi, akisema sekta hiyo pekee haiwezi kuwa tegemeo la maisha kwa muda wote..

“Udereva wa bodaboda una mwisho, kwa hiyo ni muhimu kijana akawa na ujuzi mwingine utakaomsaidia katika maisha yake. Chuo hiki kinatoa fursa hiyo kwa vijana kupata taaluma mbalimbali,” amesema Mhe. Shingo.

Amesema kuwa amefurahishwa na uwepo wa chuo hicho ndani ya Jimbo la Ukonga na kueleza kuwa ataendelea kuhamasisha vijana kupata mafunzo ya ufundi na ujuzi.

Kwa mujibu wa Shingo, tayari vijana takribani 700 wanaendelea na mafunzo kupitia ufadhili unaotokana na Mfuko wa Jimbo, fedha zake binafsi pamoja na mchango wa marafiki.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Future World Vocation Institute, Robert Mkola, amesema kuwa chuo hicho kinalenga kuwapatia vijana ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kupunguza utegemezi wa ajira za kuajiriwa

Mkola amesema kuwa bado kuna idadi kubwa ya vijana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari ambao huingia moja kwa moja katika shughuli za bodaboda bila kupata fursa ya kujifunza fani nyingine za kuwawezesha kujitegemea.

Mkola amewataka vijana hao kutumia fursa za elimu ya ufundi kujifunza fani mbalimbali, akisisitiza kuwa kuwa dereva wa bodaboda kunaweza kuwa sehemu ya maisha, lakini si lazima iwe ndiyo taaluma pekee ya kijana.

“Tunataka vijana wajenge uwezo wa kujiajiri. Hatuwezi kuwa na kizazi ambacho vijana wote wanaishia kuwa waendesha bodaboda bila kuwa na ujuzi mwingine wa kuwawezesha kujitegemea,” amesema.

Amesema chuo hicho kinaendelea kutoa mafunzo katika fani mbalimbali, ikiwemo udereva, urembo na malezi ya watoto, huku kikitumia mbinu za kisasa katika ufundishaji.

Post a Comment

0 Comments