Header Ads

ad728
  • Breaking News

    THBUB yawafikia zaidi ya wananchi 89,000 kupitia elimu ya haki za binadamu




    Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeendelea kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa kuwafikia zaidi ya wananchi 89,000 kupitia njia mbalimbali za utoaji elimu katika mwaka wa fedha 2025/2026.

    Elimu hiyo ilitolewa kupitia mafunzo kwa makundi mbalimbali ya jamii, vipindi vya redio na televisheni, mitandao ya kijamii, huduma ya ujumbe mfupi wa simu (Bulk SMS) pamoja na usambazaji wa vipeperushi na machapisho ya elimu.

    Taarifa hiyo imetolewa na Msemaji wa Tume hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Mawasiliano,Utafiti na Nyaraka wakati akiongea na vyombo vya habari katika viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara saba saba leo Juni 29,2029

    Bi. Mnanka amesema katika kipindi hicho, wananchi zaidi ya 80,000 walifikishiwa ujumbe wa elimu kupitia simu za mkononi, huku vipeperushi 39,129 na vitabu 200 vya elimu vikisambazwa kwa wananchi ili kuongeza uelewa kuhusu haki za binadamu, utawala bora na namna ya kuwasilisha malalamiko THBUB.

    Aidha, Tume ilirusha vipindi 79 vya elimu kupitia redio na televisheni, hatua iliyochangia kuwafikia wananchi wengi zaidi nchini.

    THBUB imesema itaendelea kutumia teknolojia na majukwaa mbalimbali kuhakikisha elimu ya haki za binadamu inawafikia Watanzania wengi zaidi.

    Pia, Bi. Mnanka amesema THBUB imeendelea kuwekeza katika elimu ya haki za binadamu kwa kutoa mafunzo kwa zaidi ya washiriki 9,300 kutoka makundi mbalimbali ya jamii nchini katika mwaka wa fedha 2025/2026.

    Akitoa takwimu ya walionufaika na mafunzo hayo, Bi. Mnanka ametaja makundi hayo kuwa ni pamoja na askari wa Jeshi la Polisi 827, waandishi wa habari 324, madiwani 60, wanafunzi zaidi ya 8,000 na walimu 121 kutoka vyuo vikuu tisa pamoja na taasisi nyingine za elimu.

    Mafunzo hayo yalilenga kuongeza uelewa kuhusu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na wajibu wa kila mmoja katika kulinda na kuheshimu haki hizo.

    “…..kuwajengea uwezo makundi mbalimbali katika jamii ni hatua muhimu ya kuimarisha utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu na kuzuia vitendo vya uvunjifu wa haki na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora…..” amesema Bi.Mnanka.

    No comments