Akizungumza Mkoani Mtwara katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo, Mhe. Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha Wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi wanapata umeme wa uhakika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, ameipongeza ETDCO kwa kuendelea kutekeleza miradi ya umeme kwa wakati na ufanisi mkubwa.
Mhandisi Mramba amesema Serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo mradi wa laini ya Kusafirisha umeme wa Masasi - Mahumbika wa msongo wa kilovolti 220, ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema mradi huo wa laini ya msongo wa kilovolti 33 wenye urefu wa takribani kilomita 76 utaboresha upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Newala na kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme.
Ameongeza kuwa TANESCO inatarajia kutekeleza mradi wa shilingi bilioni 5.27 wa ujenzi wa kituo kipya cha kupooza umeme (Switching Station) Wilayani Newala ili kuimarisha zaidi huduma ya umeme.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu Kampuni ya ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja, amesema Kampuni imefanikiwa kukamilisha mradi huo wenye urefu wa takribani kilomita 76 ndani ya miezi saba badala ya miezi 12 iliyokuwa imeainishwa kwenye mkataba.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, Mhe. Dkt. Yahya Nawanda, ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 4.6, akisema utachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi kupitia Sekta za Viwanda, Kilimo na Ajira katika Wilaya hiyo.
Nao wakazi wa Wilaya ya Newala wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo, wakieleza kuwa utaimarisha shughuli za uzalishaji, kukuza uchumi na kuharakisha maendeleo ya wananchi



0 Comments