Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 18, 2026, jijini Dar es Salaam.
..........
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026, huku ikitoa angalizo kuwa msimu huo utaathiriwa kwa kiwango kikubwa na El Niño yenye nguvu inayotokana na joto la bahari kuwa juu ya wastani katika Bahari ya Pasifiki, jambo linalotarajiwa kuchangia ongezeko la mvua za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 18, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa msimu wa Vuli 2026 unatarajiwa kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na El Niño, hivyo mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo yaliyotajwa.
Dkt. Chang’a amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya Septemba hadi wiki ya kwanza ya Oktoba 2026 katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria, kabla ya kusambaa taratibu katika maeneo mengine mwezi Oktoba.
Kwa kawaida, mvua za Vuli huisha mwezi Desemba, hata hivyo, katika msimu huu, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea hadi Januari 2027, huku ongezeko kubwa likitarajiwa hasa mwezi Novemba 2026.
Akielezea athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a ametahadharisha kuwa unyevunyevu uliokithiri kwenye udongo pamoja na mafuriko vinaweza kutokea na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.
Aidha, ongezeko la kina cha maji katika mabwawa na mito linaweza kuathiri miundombinu ya rasilimali za maji na nishati, huku uchafuzi wa maji ukiongeza hatari ya milipuko ya magonjwa.
Pia, magonjwa ya mazao yanayosababishwa na kuvu, bakteria na virusi yanaweza kuathiri uzalishaji wa viazi mviringo, alizeti, maharage, ufuta, matunda na mbogamboga.
Sekta za usafiri, ujenzi na utalii nazo zinaweza kukumbwa na changamoto ikiwemo barabara, uharibifu wa madaraja na kuhama kwa wanyamapori kutokana na mafuriko.
Dkt. Chang’a amewashauri wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

0 Comments