Katika kuhakikisha ulinzi wa wanawake unaimarishwa, Taasisi ya Pastoral Women’s Council (PWC) ya Mkoa wa Arusha imesema inaendelea kuhamasisha na kusambaza Agenda ya Wanawake, Amani na Usalama, kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.
Hayo yamesemwa leo, Septemba 8, 2026, jijini Dar es Salaam na mwakilishi wa Jumuiya ya Wanawake Wafugaji Mkoa wa Arusha, Nalemuta Moisan, ambaye amesema taasisi hiyo imekuwa ikitoa mchango katika kuwawezesha wanawake kushiriki katika masuala ya uongozi, pamoja na kuwapatia fursa mbalimbali katika sekta ya kilimo na maeneo mengine ya kiuchumi.Amesema suala la ulinzi wa wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia limepewa kipaumbele, huku taasisi hiyo ikiendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Agenda ya Wanawake, Amani na Usalama.
“Agenda ya Wanawake, Amani na Usalama ni azimio muhimu katika kujenga fursa kwa wanawake. Tumekuwa tukishirikiana na Serikali katika kutekeleza agenda hii, ikiwemo katika utatuzi wa migogoro,” amesema Nalemuta Moisan.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Global Peace Foundation (GPF), Hussein Faraji, amesema Agenda ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2035 imeendelea kutoa msisitizo katika masuala ya ulinzi na usalama wa wanawake.
Amesema Tanzania, kutokana na kupakana na nchi mbalimbali, imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohusiana na ulinzi na usalama, ikiwemo changamoto za ulinzi wa haki za wanawake katika baadhi ya maeneo, kama Mkoa wa Kigoma.
Hussein amesema bado kuna changamoto katika kuhakikisha ajenda za kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake zinatoka kwenye nyaraka na kwenda katika utekelezaji wa vitendo.
“Hatua hii imekuwa ngumu sana katika kupambana na changamoto ya ukatili dhidi ya wanawake, hasa katika kuhakikisha masuala yaliyo kwenye makaratasi yanafanyiwa kazi na kutekelezwa kwa vitendo,” amesema Mkurugenzi huyo.

0 Comments