Na Francisco Peter, Dar es Salaam
Shirika la Reli Tanzania (TRC) lipo katika hatua za usanifu wa kutengeneza mabehewa maalum yatakayokuwa na vifaa vya matibabu na vitanda kwa ajili ya kutoa huduma za dharura, maarufu kama “ambulance ya treni”.
Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kimkakati unaotekelezwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ambapo taasisi hizo zimetangaza ushirikiano utakaowawezesha abiria wanaosafiri kwa treni ya kisasa ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma kupata huduma za uchunguzi na vipimo vya afya ya moyo bila malipo.

Akizungumza katika Stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kissenge, amesema kuanzia Septemba 21 hadi 27, wataalamu na mabingwa wa afya watasafiri ndani ya treni za SGR kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo pamoja na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza kwa abiria watakaopenda kupimwa.
Dkt. Kissenge amesema huduma hizo zitatolewa bure ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka Septemba 29.
“Vipimo hivi vyote, vikiwemo Echo, ECG, vipimo vya sukari na mafuta kwenye damu, vikifanyika hospitalini vinaweza kugharimu zaidi ya Shilingi 500,000.
Hata hivyo, katika kipindi hiki cha wiki ya afya ya moyo, abiria wote watapata huduma hizi bure kabisa wakiwa safarini,” amesema Dkt. Kissenge.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Masanja, amesema ushirikiano huo ni mwanzo wa mpango mpana zaidi wa kimkakati katika utoaji wa huduma za afya kupitia usafiri wa reli.
Amesema mabehewa hayo maalum yatakapokamilika yatawezesha pia kusafirisha wagonjwa mahututi na wanaopewa rufaa kutoka mikoani kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili au hospitali nyingine kuu kwa haraka na kwa usalama zaidi.
“Mabehewa haya yatasaidia sana kupunguza muda wa kusafirisha wagonjwa waliopo katika hali mbaya kutoka mikoani, kama Dodoma na Morogoro, ikilinganishwa na kutumia magari ya dharura (ambulance) ya barabarani,” amesema.
Aidha, Mhandisi Masanja amesema mpango huo wa mabehewa ya matibabu unatarajiwa kuanza kutekelezwa ndani ya miezi sita ijayo.
Viongozi hao wametoa wito kwa wananchi na abiria wote wanaosafiri kwa treni za SGR katika kipindi hicho kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo kupima na kuchunguza afya zao.
0 Comments